Kheri ya Siku Kuu na Mwaka Mpya

Mpendwa msomaji,

kwa maneno haya machache ninapenda kukushukuru kwa kusoma machapisho yetu na kukutakia kheri ya siku kuu na mwaka mpya wenye afya na baraka katika kutimiza njozi na mipango yako.

Iwapo ni mara yako ya kwanza kuingia katika ukurasa huu, tafadhali jipatie wakati mfupi na kupitia machapisho yalioandikwa hapo chini. Tutafurahi kupokea maoni yako.

Machapisho haya yamelenga kutia moyo vijana katika safari yao ya kujiendeleza kimasomo na kiuchumi, na kuwahabarisha katika mada kadha wa kadha, k.v. namna ya kufungua biashara, vidokezo kuhusiana na namna ya kujiendeleza kielimu, kumudu mapato binafsi n.k. Iwapo kuna mada unayotamani tuiwasilishe hapa na inayoweza kuwa na manufaa kwa vijana, usisite kutuandikia. Pia usisite kujulisha wengine kuhusu tovuti/blogu hii ili pia hata wao waweze kufaidika.

Tunatarajia mwakani, tutakapokuwa na wasomaji wa kutosha, kufungua jukwaa la majadiliano (forum) kuhusiana na mada tunazihudumia katika tovuti yetu. Kwa taarifa zaidi kuhusu mada zetu, angalia hapa. Jukwaa hili husaidia wadau kubadilishana mawazo, kufahamiana, na kujitengenezea mtandao wa kusaidiana katika mada husika (kwa mfano fursa za mafunzo maalumu, upatikanaji wa kazi n.k.). Iwapo una shauku, jiskie huru kujiunga kupitia fomu hii. Tutakujulisha hatua zinazoendelea, na baada kupokea watu wa kutosha, tutalifungua jukwaa hilo la mawasiliano.

Nabaki kukutakia kila la kheri katika siku kuu na mwaka mpya, mapumziko mema ya shughuli na baraka tele katika kutimiza malengo mapya katika mwaka unaokuja.

 

Namna ya kumudu gharama zako za maisha

Nani havifahamu vipindi vya hali ngumu kiuchumi ambapo unajikuta kipato chako hakitoshi kutekeleza mipango ulionayo au hata matumizi yako ya muhimu. Hasa pale dharura zinapozitokeza, k.v. matibabu, uharibifu wa mali za msingi au kupoteza kazi/kutolipwa mshahara, ni rahisi kujikuta katika changamoto kubwa ya kukidhi mahitaji binafsi. Mtu mwenye utamaduni wa kujiwekea akiba ya kutosha hata kuweza kumudu kipindi cha miezi kadhaa cha dharura au mtu mwenye vipato mbadala kutoka katika miradi mingine anaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kumudu dharura hizi huku akiendeleza mipango yake ya maisha na ya maendeleo. Kwa sababu si wote walio na akiba au miradi hii, lazima tutazame njia zingine za kuweza kumudu gharama za maisha ambazo zaweza kufungua njia mbadala za kujihakikishia akiba. Ili kurahisisha usomaji, nimeyafupisha mawazo yangu katika dondoo zifuatazo.

  1. Bainisha matumizi au mahitaji yako ya msingi na yasiyo ya msingi. Aina na kiwango cha matumizi hutofautiana mtu na mtu, sehemu anapoishi na shughuli za uchumi anazofanya. Kwa mfano, matumizi ya mwajiriwa anayeishi kwenye nyumba ya kukodi jijini Daressalaam na kutumia usafiri wa daladala kila siku kwenda kazini ni tofauti na mjasiriamali nje ya jiji la Mwanza, anayeishi kwenye nyumba yake yenye bustani au shamba. Lisha ya tofauti hizo, matumizi yafuatayo yanaweza kukupatia mwongozo wa kupata picha ya matumizi yako: (i) Chakula, (ii) Kodi ya Nyumba, (iii) Nishati, kama vile umeme, gesi, mkaa, (iv) Gharama za Shule/Karo, (v) Mavazi, (vi) Usafi binafsi, k.v. Sabuni na vipodozi, (vii) Vifaa vya nyumbani, (viii) Bima ya afya, (ix) Mengineyo (nauli, mawasiliano, michango, burudani n.k.).

Unaweza kufupisha au kurefusha orodha hii kulingana na mahitaji yako binafsi. Kubainisha gharama halisi ulizonazo kila mwezi hukusaidia kuyaoanisha na mapato yako ya mwezi na kuhakikisha unamudu mahitaji na majukumu yako ya msingi bila shida huku ukiendelea na mipango yako ya kimaendeleo. Iwapo una mipango ya kuwekeza mahala fulani au kujikusanyia mtaji, pesa inayobaki kutoka kwenye matumizi unaweza kuitenga kila mwezi bila kuathiri hadhi au kiwango chako cha maisha. Ni wazi kuwa, kama kipato chako hakitoshi kukidhi mahitaji ya msingi, huna budi kutathmini matumizi yako na kuyapunguza au kutafuta kazi yenye kipato kinachoendana na gharama zako za maisha.

  1. Weka Akiba kwa ajili ya dharura. Dharura haipangwi, bali hujitokeza yenyewe. Na kuna dharura zinazokulenga moja kwa moja, ambazo hauwezi kukwepa, kama vile matibabu, uharibifu wa mali au kupoteza kazi/kipato. Akiba hii, ambayo hukadiriwa kuwa sawa na kipato chako cha miezi mitatu mpaka sita, ni tofauti na pesa unayoitenga katika kuwekeza katika biashara. Hii ni kwa sababu biashara yako ikiyumba, inaweza kukulazimu uchukue pesa kutoka katika mahitaji yako ya msingi na hivyo kushindwa kumudu gharama za maisha. Njia mojawapo ya kukwepa ukali wa dharura ni kuwa na Bima ya afya. Kutegemea na aina ya kifurushi utakachochukua, bima ya afya inakuwezesha kupunguza hatari ya kuichumi inayotokana na dharura ya kuugua. Kwa kulipia bima ya afya kutokana na pesa uliyoipangalia kwenye matumizi yako kila mwezi, unapata matibabu bila ya kuathiri akiba yako. Kwa mtu mwenye familia au mwenye ndugu anayehitaji matibabu ya mara kwa mara, kulipia bima ya afya sio tu ni kuwekeza kwenye afya bali ni tendo lenye uwajibikaji mkubwa, hasa katika dharura ya matibabu au pale unaposhindwa kulipia matibabu makubwa. Kulingana na utafiti wa FInscope (2017), matumizi ya matibabu yanashika nafasi ya tatu kwa umuhimu (baada ya gharama za kuishi, yaani chakula, kodi/malazi) na dharura ya kiafya/matibabu ni sababu namba moja ya watu kokopa pesa na kuingia kwenye madeni.
  2. Kuwa jasiri kuwekeza. Kuwekeza husaidia kujiongezea uwezo wako kuichumi na hukusaidia kutimiza malengo yako nje ya mahitaji yako ya kila siku. Sio kila mtu anaweza kuwa mfanya biashara mashuhuri, hasa ukiwa umeajiriwa wakati huo huo (kumbuka: ni hatari kuacha ajira iwapo biashara yako haikupi kipato cha kutimiza mahitaji ya kila siku). Tambua kipaji chako na wekeza katika talanta yako kupitia shughuli unayoiwezea vizuri. Badala ya biashara, unaweza kuboresha au kukuza bustani/shamba lako na ukajipunguzia gharama za chakula, kupata akiba ya chakula au hata kuuza na kupata fedha kwa ajili ya mipango mingine. Wengine hufuga, wengine husuka, wengine hujenga vibanda au nyumba kwa ajili ya kupangisha. Mianya ni mingi unapopata nafasi ya kujihabarisha na kubadilishana mawazo na watu. Walisiliana nasi pia kwa mawazo zaidi.

Kuna usemi usemao: „Mtu hula kulingana na urefu wa kamba yake“. Kuna hekima katika kutathmini matumizi binafsi, kujiongezea uwezo wa kipato, bila kuhatarisha mahitaji binafsi au ya familia, na kukwepa mikopo au utegemezi. Baadhi ya watu wanamudu hili jambo bila shida, wengine hupata ugumu. Iwapo unahitaji msaada zaidi, kimawazo au ushauri, usisite kujereja kwetu kupitia mawasiliano yalioko mwishoni mwa ukurasa huu. Tutafurahi sana   kukusaidia.

Barikiwa.

 

Bibliografia

Finscope Tanzania (2017). Insights that drive Innovation. https://www.fsdt.or.tz/wp-content/uploads/2017/09/Finscope.pdf

 

Namna ya Kufanikiwa katika Biashara Unayoianzisha

Kuanzisha biashara Tanzania huambatana na changamoto kadhaa kama ukosefu wa mtaji na mkakati dhaifu wa uuzaji. Lakini badala ya kuangalia sababu zinazofanya biashara kushindwa, napenda tujikite katika makala hii kwenye mambo yanayoweza kufanikisha biashara inayoanzishwa. Mawazo haya nimeyagawanya katika dondoo zifuatazo.

Tazama biashara za maeneo jirani unayoishi au biashara za watu unaowafahamu. Je, ni mambo gani yaliyofanya biashara hizo kufanikiwa, kubaki vilevile kwa muda mrefu, au hata kushindwa? Ni sababu zipi zimeleteleza matokeo hayo?

Kwa hakika kuna sababu nyingi,  zikiwemo sababu binafsi ambazo ziko nje ya uewelewa wetu. Kwa msingi huo hatuwezi tukadai kujua sababu za kila biashara kushindwa. Hata hivyo, napenda tutazame baadhi ya mambo muhimu yanayopelekea biashara kufanikiwa au hata kushindwa.

  1. Mkakati dhabiti wa uuzaji. Watanzania wanafahamu kutumia fursa katika kufanya biashara zao. Hii huusisha kufungua biashara katika maeneo yalio na watu wengi, au karibu ya kaya zao ambapo wanaweza kuduhumia kaya za jirani kwa bidhaa na huduma huku wakitimiza majukumu yao ya nyumbani. Popote pale biashara yako ilipo, ili ikue na ifanikiwe, inapaswa kujikita katika kutimiza hitaji flani la watu walioko katika eneo hilo.  Hivyo shauku ya kuanzisha biashara na kujishughulisha haina budi kuambatana na mahitaji ya msingi ya watu katika eneo husika. Ili kuweza kujua mahitaji ya wateja wako wa baadaye na kufanya uamuzi mzuri wa aina ya biashara ya kuendesha, unapaswa kufanya utafiti wa soko.
  2. Naamini unafahamu tabia ya baadhi ya watu kuelekea katika fursa flani ya biashara na kubadili mwelekeo, yaani biashara, pale wanapoona fursa nyingine. Ni kweli kuwa kupata uzoefu katika biashara tofauti tofauti huleta manufaa. Hata hivyo, swala la kubadili badili biashara lapaswa kutathminiwa kwa kina, hasa pale ambapo matokeo yake yanaathiri kipato cha familia. Kwa hakika jambo hili tunalitazama kwa utofauti, iwapo mtu ana kipato thabiti kutokana na ajira, chenye kukidhi mahitaji yake na familia yake huku “akijijaribu” katika biashara flani. Kutimiza wajibu wa riziki yako na familia yako ni muhimu huku ukijikita katika biashara yako kwa uvumilivu na kutafuta mafanikio katika biashara hiyo.
  3. Udhibiti mzuri wa mtaji. Nimekutana na baadhi ya wanafanyabiashara wanaotumia pesa au bidhaa za biashara kwa ajili ya matumizi yao binafsi (k.v. kwa ajili chakula, nauli au dharura). Hili jambo, hata kama wakati flani halikwepeki, linahitaji nidhamu kubwa. Ikarimu unaweza kuhatarisha biashara yako. Kutenganisha matumizi ya biashara na matumizi binafsi ni jambo la msingi sana. Ni kweli kuwa upatikanaji wa mtaji ni muhimu katika kuanzisha biashara. Mtu achukuaye mkopo kwa ajili ya mtaji anapaswa kutuambua deni analodaiwa na umuhimu wa kulipa deni hilo, ukizingatia kuwa kipindi cha awali cha biashara huwa kinaambatana na hasara. Kiasi kikubwa cha mkopo humaanisha pia kiasi kikubwa cha deni na kiasi kikubwa cha deni huweza kupelekea kushindwa kulipa kama pesa haidhibitiwi vizuri au ikijitokeza hasara kubwa kutoka na mauzo au wizi. Kama unakusudia kuanzisha biashara ndogo, fikiria kuhusu biashara zisizohitaji mtaji au zinazohitaji mtaji mmdogo. Kumbuka methali inayosema: “Mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe” . Jipatie mawazo kupitia mtandao au marafiki kuhusu aina za biashara zisizohitaji mkopo au zinazohitaji mkopo mdogo. Unaweza kuwasiliana nasi kwa mawazo zaidi.
  4. Jifunze kuboresha biashara yako. Kimsingi, ni vema kupata maarifa ya biashara hata kabla ya kuanza biashara. Unaweza kuona wepesi wa kufanya biashara, lakini kuwa mnyenyekevu ili kujifunza zaidi na kuepuka makosa ya kibiashara, kunaweza kukusogeza mbele zaidi. Kama umeshaanza biashara yako, jipatie muda, utoke katika mihangaiko ya biashara yako, ili ujifunze namna ya kuiboresha. Kutana na wanafanyabiashara wengine wazoefu zaidi na waliofanikiwa, pata ushauri kutoka benki, jiunge katika jukwaa la majidala au tafuta mshauri wa kitaalam ili ujifunze kutokana na uzoefu wa wengine na changamoto zao. Unaweza kufaidika sana.

Je, kuna mambo mengine ya kuzingatia katika kuendesha biashara? Tafadhali tushirikishe. Kama una swali au haja yoyote, jiskie huru kuwasiliana nasi. Kama inahitaji kufahamu zaidi kuhusu uendeshaji wa biashara, jipatie nyenzo hapa.

Nakutakia kila la kheri katika biashara yako

Umuhimu wa Kujiendeleza Kielimu

Kazi nyingi siku hizi zinahitaji elimu, iwe ni kwa mtu anayeingia soko la ajira, au anapoanza biashara, au kwa mtu anayehitaji kuboresha utendaji wake katika taaluma au kazi anayoifanya. Hata hivyo, kutokana na ushindani uliopo katika soko la kazi na mategemeo yaliyowekwa katika ubora wa utendaji kazi, haina budi kila mtu kujiendeleza kitaaluma. Mtu aliyesoma, kubobea katika taaluma yake, na kujipatia uzoefu wa kazi hata  katika kipindi cha uanafunzi katika kujitolea mahali, ana fursa kubwa ya kujitengenezea riziki kwa ajili yake na familia yake. Katika ngazi zote za elimu, Tanzania inatoa fursa ya kujiendeleza kielimu na kubobea katika fani au taaluma. Jedwali lifuatalo linaonesha baadhi masomo ya taaluma tofauti tofauti katika kiwango cha cheti na stashahada. Asilimia kubwa ya kozi hizi huweza kusomwa na mtu aliyehitimu elimu ya sekondari (kidato cha nne). Jedwali hili ni mfano tu unaoweka bayana kuwa kila mtu (katika kiwango chake cha elimu) anaweza kujiendeleza na kubobea katika taaluma anayopenda. Tofauti na kuanza moja kwa moja na elimu ya cheti au stashahada, kuna uwezekano wa bobea kwenye taaluma kupitia VETA, shahada au hata kozi fupi zinazotelea na taasisi tofauti tofauti za elimu. Kama una maswali zaidi au unahitaji ushauri kuhusiana na kujiendeleza kielimu, wasiliana nasi kupitia mawasiliano yetu yalioko upande wa chini wa ukurasa huu. Ili kuziona kozi ya cheti na stashahada, bonyeza hapa.

Mwongozo wa Usajili wa Biashara kwa Mitaji Midogo na Mikubwa

 

Unatamani kuanzisha biashara yako ili uweze kutimiza njozi yako ya maisha na kujitegemea kiuchumi?

Ni dhahiri kuwa sio kila mtu anaweza kufanya biashara yoyote. Huenda umesha litafakari hili na kufanya tathmini kuhusu aina ya biashara inayoendana na uwezo na karama yako. Huenda pia umeshajipatia uzoefu katika biashara yako hiyo na kutathmini soko lake. Kama sivyo, usisite kuwasiliana nasi ili tuweze kuangalia kwa pamoja ni biashara ipi inaweza kukufaa na nambna ya kijipatia taarifa na mafunzo muhimu kwa ajili ya biashara hiyo.

Waraka huu unakusudia kukupatia mwongozo mfupi wa hatua unazopaswa kuzichukua kabla ya kuanzisha biashara yako. Hii inakusaidia kuzingatia miongozo muhimu ya kisheria ili kuweza kuanzisha biashara yako iliyo rasmi, itakayokufungulia milango ya huduma zingine maalumu, k.v. mkopo wa benki, mafunzo, na mtandao wa wafanyabiashara wengine. Hata hivyo waraka huu unakusaidia kukupa tathmini fupi ya gharama zinazohusika katika kupanga na kuanzisha biashara yako.

Hatua za uanzishaji wa biashara:
– Hatua ya kwanza ni lazima ujue aina ya biashara unayohitaji kuanzisha, ikiwemo na rasilimali husika (k.v. ofisi, pikipiki, elimu husika/cheti, bima n.k.). Uamuzi wa aina ya biashara huhusisha pia uamuzi kama biashara hiyo itaendeshwa kama biashara ya mtu binafsi, ubia au kampuni yenye dhima ya ukomo

– Hatua ya pili ni kusajili jina la biashara yako katika ofisi ya BRELA (Mamlaka ya Usajili wa Biashara na Leseni). Gharama utakayolipa kwa ajili ya hati ya usajili ni Tsh. 20 000/-

– Hatua ya tatu ni kupata namba ya mlipakodi (TIN). Namba hii utaipata katika ofisi ya TRA ya Mkoa au Wilaya baada ya kujaza fomu ya maombi ya namba ya utambulisho wa mlipakodi. Namba ya TIN ni bure, ila utalipia ushuru kutokana na makadirio yako ya mapato ya mwaka huo au mtaji wako uliowekeza katika biashara

– Hatua ya nne ni kujipatia leseni ya biashara katika ofisi za biashara katika wilaya, manispaa, jiji au wizara ya biashara na viwanda. Gharama ya leseni hutegemea aina ya biashara unayohitaji kuanzisha. Gharama hii utaijua katika ofisi hiyo ya biashara. Kutazama fomu ya maombi ya leseni, bonyeza hapa.

Bajeti ya gharama zote za kupitia hatua hapo juu ili kuanzisha biashara ya mtu binafsi (kwa mfano) hukadiriwa kuwa shilingi laki tatu (Tsh. 300 000/-). Kwa mtu ambaye hana uwezo wa kulipa hii pesa, anashauriwa kurejea katika mfumo wa wafanyabiarasha/wajasiriamali wadogo na kujipatia kitambulisho kutoka katika ofisi za TRA kabla ya kuanzisha biarasha yake. Ili kuweza kufanikisha ili, unapaswa kuanzia na taratibu husika katika serikali zako za mitaa. Jifahamishe katika eneo unaloishi kuhusiana na uwepo wa mifumo hii vikundi au umoja wa biashara fulani fulani zinazoweza kukupatia msaada zaidi. Fomu ya maombi ya kitambulisho cha mjasiriamali unaweza kuipakua hapa. Gharama ya kitambulisho cha mjasiriamali mdogo ni Tsh. 20 000/-

Kama una swali ama unahitaji mwongozo zaidi, usisite kuwasiliana nasi kupitia info@societalnurturing.com au 0784462140