Timiza Ndoto Zako kupitia Biashara

Kuanzisha na kuendesha biashara inayopendwa na yenye mafanikio ni shauku ya vijana wengi. Changamoto katika kuanzisha, kuendesha na hata kuimarisha biashara tunazifahamu. Swala la kuendesha biashara limekuwa schangamoto kwa wengi kiasi kwamba wengi wanaofanikiwa kuendesha biashara, wameshindwa kujikimu kimaisha kutokana na mapato duni ya biashara zao. Takwimu zilizotolewa na Shamchiyeva, Kizu na Kahyarara kupitia shirikia la kazi duniani (ILO) linaonesha wastani wa mapato ya vijana wa kiume ni Tsh. 117,000/= kwa mwezi na kwa vijana wa kike ni 90,000/=. Japokuwa hizi takwimu zina miaka karibia kumi sasa, hata kama wastani umepanda kwa sasa ukilinganisha ni kipindi cha utafiti, haitoshi kujikimu kimaisha. Ukipiga hesabu ya pesa mtu anayohitaji kijikumu kimaisha kwa (ikihusisha chakula, kodi, usafiri, mawasiliano, afya na huduma tofauti tofauti – hata kama zinatofautianana maeneo na maeneo) lazima kiwango kisipungue laki tatu.

Wakati vijana wengi wakitafuta uhuru wa kiuchumi, kujitegemea na kuongeza kipato kupitia biashara, asilimia yao kubwa huingia kwenye biashara kwa sababu ya kukosa ajira. Changamoto hii huambatana na vijana wengi kutopangilia biashara yao vizuri – kuanzia kulenga wateja, mipango ya biashara ya muda mfupi na mrefu, na utekelezaji wa biashara hizo, kama Isai Mathias anavyoweka wazi katika waraka wake kuhusu sababu ya biashara  nyingi kufeli. Changamoto zinigine kama ukosefu wa mtaji, elimu, na uzoefu, mikopo yenye riba kubwa, upanuaji wa biashara kwa pupa, matumizi ya pesa ya biashara kwa ajili ya mahitaji binafsi, eneo baya ya biashara, na uendeshaji duni tunayafahamu.

Wakati huo huo tunafahamu kuwa uanzishaji und uendeshaji wa bia biashara – hasa kwa Tanzania ambapo mazingira huruhusu na sheria hazibani, ni fursa kubwa ya kufanya mambo na kutimiza ndoto binafsi.

Tunatambua kuwa sio kila mtu anaweza kuendesha biashara. Sio kila mtu atakuza biashara. Unaweza kutathmini uzuji/uwezo ulionao, sifa binafsi (k.v. motisha, hali ya uchumi), athari zinazoweza kujitokeza, na hali halisi, na kuchagua biashara inayokidhi mahitaji ya watu unaowalenga. Sifa hizi unaweza kujipatia. Kama unahitaji mwongozo zaidi katika kuanzisha biashara yenye mafanikio na inayoendana na mazingira uliyonayo, usisite kuwasiliana nasi. Kama unahitaji kuhudhuria mafunzo na kujijengea sifa kwa ajili ya biashara bora, usisite pia kuwasiliana nasi.

Fursa za Kujiajiri Tanzania

Lengo la makala hii ni kukuwezesha kuanza biashara mara moja na kuifanikisha,  iwapo utaamua. Hivyo karibu uisome makala hii mpaka mwisho.

Kama inavyofahamika, swala la mtaji, ujuzi, usimamizi mzuri na kutambua/kutengeneza fursa ni misingi muhimu katika uendeshaji wa biashara. Mara nyingi biashara zinakwama katika msingi hii.  Hebu tafakari jambo hili:

Fundi anapokuwa anashidwa kuhakikisha kazi ya mteja imefanyika wa uzuri na kwa wakati, huathiri kipato chake na ukuaji wa biashara yake. Mategemeo ya faida ya haraka na ukosefu wa nidhamu katika matumizi ya pesa ya biashara, hupelekea kutumia sehemu ya pesa ya biashara katika mahitaji binafsi (k.v. matibabu, chakula, ada ya shule) au hata kupunguza kuwekeza muda wa kutosha katika biashara. Katika mazingira haya, biashara hubaki kuwa duni.

Huenda umeshafirikia ni biashara gani ungependa kuianzisha na vigezo unavyohitaji kuvitimiza ili kufanikisha biashara hiyo. Umetathimini soko na kuona kuna fursa au uhitaji mkubwa ya bidhaa au huduma unayotaka kuitoa na pesa unayolenga kuipata. Kanuni iongozayo ni uhitaji wa bidhaa au huduma yako. Kama hakuna uhitaji mkubwa, hiyo biashara haiwezi ikajiendesha na kukidhi mahitaji yako. Panapokuwa na uhitaji mkubwa, una uhakika wa wateja. Wakati mwingine inakuhitaji kujihakishia wateja wa awali na kuwa na mzunguko mdogo wa pesa ili kuimarisha biashara yako, kabla haujabobea katika hiyo biashara na kuwekeza muda na pesa zaidi, au hata kusitisha shughuli zako zingine.

Biashara nyingi zinahitaji mtaji, ila sio zote. Kwa mfano biashara zinazotumia ujuzi wako na sisizohitaji ofisi kama, kufundisha au kusuka, hazihitaji mtaji. Hivyo, tafakari kuhusu gharama unazoweza kuziepuka katika kuanzisha biarashara yako.

Ujuzi wa kazi katika bishara ni muhimu. Mwalimu anayefundisha shule haitaji kufahamu utaratibu wa makato ya serikali, vibali na gharama za uendeshaji, namna ya kupata na kuwafikia wateja na kutengeneza mfumo mzuri wa uendeshaji wa kituo au kutengeneza mikataba. Mwalimu anayeendesha kituo cha tuisheni kwa upande mwingine hupaswa kufahamu haya. Hivyo unapoanzisha biashara yako, tafakari kuhusu mambo unayopaswa kuyajua kabla ya kuanza.

Je, katika biashara unayokusudia na una ujuzi wa kutosha? Unahitaji ujuzi kuhusu namna ya kujipatia wateja na kukuza biashara yako kupitia mtandao? Ni kweli, si lazima ujue kila kitu ili uanze biashara ila unapaswa kutambua mipaka yako katika kufikia malengo uliyoweka. Kupitia mafunzo, marafiki, washauri au hata wafanyabiashara wenza, unaweza kuziba hilo pengo.

Ili kufikia malengo, usimamizi unapaswa kuwa mzuri. Usimamizi huusisha mipango ya muda mfupi na mrefu. Pamoja na namna ya kufikia malengo hayo, juhudi na usimamizi katika kufikia malengo hayo, watu/wafanyakazi watakaosaidia kufika malengo hayo, uongozi na ukaguzi wa kazi, pamoja na maamuzi thabiti pale ambapo malengo husika hayajafikiwa, ni mambo ya msingi ya kuzingatia.

Pale ambapo unakuwa hauko makini katika kutimiza malengo ya biashara, kutoweka mbinu za kutimiza kazi hata wakati wa dharura, lazima kutambua athari yake katika biashara na kipato chako. Unapochagua ndugu au marafiki kama wafanyakazi bila kuweka kipaumbele katika uwezo na elimu yao, bila kuzingatia mgongano wa masilahi katika kukamilisha malengo yako ya biashara na kupata ujuzi unaohitaji, ni rahisi kuwa na biashara isiyoendelea. Sio lazima kumuajiri mtu na kufanya kazi naye, ili uweze kumsaidia. Biashara nyingi za kusaidiana zinabaki katika hali ya chini, hazikidhi gharama ya uendeshaji na mahitaji. Wengi wanaishia kuomba omba na kukopa, lisha ya kuwa wana biashara. Kuna watu wanaokubali tenda ili wapate pesa ya kufanya kazi ya mteja mwingine na kupata hela ya kula. Mazingira haya yamefanya biashara zetu nyingi kuwa katika hali duni.

La mwasho – biashara nyingi hushindwa kufanyika kwa sababu ya kusingizia vikwazo vya mtaji, ujuzi au mifumo duni (sheria n.k.). Visingizio hivi havisaidii pale tunapotafuta suluhisho hata kwa kuanza taratibu.

Mfano: kama ninahitaji kufungua stationery na sina mtaji wa milioni 3 au siwezi kupata kwa ndugu/marafiki, naweza kuona pa kuanzia huku nikiweka mpango thabiti namna ya kufikia lengo hilo, hata kama likichukua muda zaidi. Naweza nikaangalia pa kuanzia kulingana na mahitaji ya wateja hali nikijua sitaweza kuitegemea hiyo biashara riziki ya kila siku. Mahitaji ya wateja yaweza kuwa madaftari, kalamu, nitanunua vitu hivyo  na kuuzia wateja huku huku nikiendelea kuzingatia mahitaji zaidi na  kukuza mtaji wangu. Naweza pia kutumia Kompyuta ya mtu kuchapa kazi za wateja. Njia hii ndefu ni uwekezaji, haupaswi kutegemewa kama riziki, lakini husadia kufikia malengo

Mfano wa pili: Kama ninahitaji pikipiki kama kitega uchumi ila sina hela, naweza

  1. Kuunganisha nguvu na mtu/watu (njia ya haraka)
  2. Kukusanya pesa taratibu kwa ajili ya pikipiki nitakayoimudu baadaye
  3. Kuchagua biashara mbadala yenye mtaji nitakaomudu, ila wenye matapo yatakayoniwezesha kuelekea kwenye hilo lengo la pikipiki

Iwapo unahitaji msaada zaidi katika kuanzisha na kushimamisha biashara yako, usisite kuwasiliana nasi.

Kumudu Changamoto katika Kujiendeleza

Swala la kujiendeleza kimasomo, kuanzisha biashara au hata kutapata kazi wakati mwingine sio jepesi. Hasa pale unapohangaika kutafuta ada, nafasi ya chuo, mtaji au ujuzi wa biashara au hata kazi inayofaa ili kutimiza ndoto na kulisha familia, changamoto hulinganishwa na kupanda mlima mkali. Ni kweli, wakati mwingine wapo ndugu na jamaa kufariji au kuwezesha kwa namna moja au nyingine. Wakati mwingine pia unalazimika kuanza kwa kiwango cha chini na kutumia rasilimali ulizonazo ili kujiendeleza, hata kama hali hairidhishi. Katika juduhi zote za kumudu changamoto hizi,  tunakutia moyo usonge mbele. Iwapo unajiona uko katika njiapanda na unahitaji msaada katika kumudu changamoto zako, jisikie huru kuwasiliana nasi. Katika kipindi cha miezi mitatu ijayo hatuzatoza gharama yoyote, maana mafanikio yako ni kipaumbele chetu. Tena, huduma yetu haishii kwenye ushauri tu, bali tunakupatia mwongozo na tutashirikiana nawe mpaka utakapofanikisha malengo yako.

Umuhimu wa Bima katika Kudhibiti Bajeti

Nani asiyeufahamu ule mzigo unaotokana na gharama za kuuguza mgonjwa katika familia au ule wa kufidia pengo, pale ambapo mwanafamilia anapokuwa amepoteza kazi au kipato?  Dharua kama hizi zinapotokea hazikwamishi tu mipango ya maendeleo bali huweza hata kuyumbisha uchumi binafsi na wa familia. Lile pengo ambalo zamani lilikuwa likizibwa na wanafamilia au ukoo katika dharura za ugonjwa, kifo, ukosefu wa kipato/mazao, au hata mahitaji mengine ya msingi sasa linaongezeka. Familia nyingi hufikia kikomo katika kujaribu kuhakikisha wanafamilia na wanaukoo wanapata huduma za msingi wanazozihitaji. Ukosefu wa matibabu au wa ada ya kusoma kwa baadhi ya watu, kuwepo kwa watoto wa mitaani/yatima au omba omba waliokosa msaada ni mifano michache inayothibitisha haya.

Mifuko ya hifadhi ya jamii husaidia kupunguza makali haya. Kwa kuchangia kiasi kidogo cha pesa, bima hizi hukusadia kuhifadhi kiwango chako cha maisha pale unaposhindwa kujihakikishia kipato ajili yako na familia yako kutokana na ugonjwa, ujauzito/uzazi, ulemavu, uzee, au kifo. Hata hivyo, mfuko huu unasaidia kutoa msaada nafuu na endelevu kwa ndugu yako kwa kumpilia gharama za uanachama, kwa sababu atanufaika pale atakapohitaji huduma ya afya.

Katika jedwali lifuatalo nimebainisha mifuko minne ya hitadhi ya jamii na huduma zake ili kukupatia taarifa za msingi zitakazoweza kukusaidia kufanya maamuzi sahihi katika kupangilia mambo yako. Hii orodha inahusisha Bima zinazopatikana nchi nzima ya Tanzania. Iwapo unahitaji taarifa zaidi kuhusiana na huduma zinazotolewa, tafadhali wasiliana na bima husika. Kama una swali kuhusiana na jedwali hili au una maoni, mapendekezo au hata nyongeza, karibu tuwasiliane. Kwa ushauri zaidi, wasiliana nasi pia.

No.Jina la BimaWalengwaHudumaGharama
1CHF (Common Health Insurance)
Bima ya Afya
WoteMatibabu yafuatayo katika vituo vyote vya serikali nchini Tanzania bara:
Ushauri wa daktari, vipimo vya maabara, vipimo vya picha (X-ray na ultra sound), dawa, kulazwa, upasuaji (wa Kawaida, Mdogo na Mkubwa), huduma za rufaa zilizopo ngazi ya mkoa.

Huduma zingine hazigaramikiwi
Kwa Daressalaam: Tsh. 40000/- kwa mwaka kwa mtu mmoja, Tsh. 150000/- kwa familia ya watu wasiozidi sita

Kwa mikoa mingine: Tsh. 30000/- kwa mwaka kwa familia isiyozidi watu sita
2NHIF (National Health Insurance)
Bima ya Afya
WoteHuduma ya Afya kama zilivyoorodheshwa katika tovuti ya NHIF, katika vituo vilivyosajiliwa na NHIF.
Huduma humlenga kwa mlipaji, mwenzi wake na watoto/wategemezi wanne
Bima ya Afya ya mtoto na wanafunzi wa chuo ni Tsh. 50400/- kwa Mwaka

Waajiriwa hulipia 6% ya mshahara.

Wengine wote kuanzia Tsh. 192 000/- kwa mwaka

Wastaafu katika sekta ya umma hawalipi chochote.
3NSSF (National Social Security Fund)
Bima ya Pensheni
Mwajiriwa katika sekta binafsi
Mjasiriamali katika sekta isiyo rasmi
Mafao ya kupoteza Ajira, 33.3% ya Msharaha kwa miezi 6

Mafao ya uzazi, 100% ya mshahara kwa miezi 3

Mafao ya Ulemavu

Msaada wa Mazishi, Tsh. 150 000/- mpaka 600 000/-

Mafao ya uzeeni kwanzia miaka 55 (75% ya Mshahara)

Mafao ya Urithi, malipo sawa na mafao ya uzeeni

Bima ya Afya
5% - 10% ya Mshahara kwa Mfanyakazi

Mjasiriamali hulipa kwanzia Tsh. 20 000/-
4PSSSF (Public Service Social Security Fund)

Mfuko wa hifadhi ya jamii/pensheni

Muunganiko wa mifuko ya Bima ifuatayo: PSPF (Public Services Pension Fund), LAPF (Local authorities Pension Fund), PPF (Parastatals Pensions Fund), GEPF (Government Employees Provident Fund)
Watumishi wa UmmaMafao ya kupoteza Ajria, 33.3% ya Mshahara kwa miezi 6

Mafao katika ugonjwa, 40% ya mshahara kwa miezi 3

Mkopo wa nyumba

Mafao ya uzeeni (hadi 75% ya mshahara)

Mafao ya urithi, 40% kwa mwenzi, 60% kwa watoto

Mafao ya ulemavu, malipo sawa na mafao ya uzeeni

Msaada wakati wa kifo
Mtumishi wa umma hulipia 5% ya mshahara, mwajiri 10%

Bibliogafia:

CHF. http://www.chf-iliyoboreshwa.or.tz/ (24.01.2021)

NHIF. https://www.nhif.or.tz/#gsc.tab=0   (24.01.2021)

NSSF. https://www.nssf.or.tz/ (24.01.2021)

NSSF. https://www.nssf.or.tz/index.php/news/nssf-na-psssf-warahisisha-huduma-kwa-wanachama-na-wananchi-kwa-ujumla (24.01.2021)

PSSSF.  https://www.psssf.go.tz/ (24.01.2021)

 

Kheri ya Siku Kuu na Mwaka Mpya

Mpendwa msomaji,

kwa maneno haya machache ninapenda kukushukuru kwa kusoma machapisho yetu na kukutakia kheri ya siku kuu na mwaka mpya wenye afya na baraka katika kutimiza njozi na mipango yako.

Iwapo ni mara yako ya kwanza kuingia katika ukurasa huu, tafadhali jipatie wakati mfupi na kupitia machapisho yalioandikwa hapo chini. Tutafurahi kupokea maoni yako.

Machapisho haya yamelenga kutia moyo vijana katika safari yao ya kujiendeleza kimasomo na kiuchumi, na kuwahabarisha katika mada kadha wa kadha, k.v. namna ya kufungua biashara, vidokezo kuhusiana na namna ya kujiendeleza kielimu, kumudu mapato binafsi n.k. Iwapo kuna mada unayotamani tuiwasilishe hapa na inayoweza kuwa na manufaa kwa vijana, usisite kutuandikia. Pia usisite kujulisha wengine kuhusu tovuti/blogu hii ili pia hata wao waweze kufaidika.

Tunatarajia mwakani, tutakapokuwa na wasomaji wa kutosha, kufungua jukwaa la majadiliano (forum) kuhusiana na mada tunazihudumia katika tovuti yetu. Kwa taarifa zaidi kuhusu mada zetu, angalia hapa. Jukwaa hili husaidia wadau kubadilishana mawazo, kufahamiana, na kujitengenezea mtandao wa kusaidiana katika mada husika (kwa mfano fursa za mafunzo maalumu, upatikanaji wa kazi n.k.). Iwapo una shauku, jiskie huru kujiunga kupitia fomu hii. Tutakujulisha hatua zinazoendelea, na baada kupokea watu wa kutosha, tutalifungua jukwaa hilo la mawasiliano.

Nabaki kukutakia kila la kheri katika siku kuu na mwaka mpya, mapumziko mema ya shughuli na baraka tele katika kutimiza malengo mapya katika mwaka unaokuja.

 

Namna ya kumudu gharama zako za maisha

Nani havifahamu vipindi vya hali ngumu kiuchumi ambapo unajikuta kipato chako hakitoshi kutekeleza mipango ulionayo au hata matumizi yako ya muhimu. Hasa pale dharura zinapozitokeza, k.v. matibabu, uharibifu wa mali za msingi au kupoteza kazi/kutolipwa mshahara, ni rahisi kujikuta katika changamoto kubwa ya kukidhi mahitaji binafsi. Mtu mwenye utamaduni wa kujiwekea akiba ya kutosha hata kuweza kumudu kipindi cha miezi kadhaa cha dharura au mtu mwenye vipato mbadala kutoka katika miradi mingine anaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kumudu dharura hizi huku akiendeleza mipango yake ya maisha na ya maendeleo. Kwa sababu si wote walio na akiba au miradi hii, lazima tutazame njia zingine za kuweza kumudu gharama za maisha ambazo zaweza kufungua njia mbadala za kujihakikishia akiba. Ili kurahisisha usomaji, nimeyafupisha mawazo yangu katika dondoo zifuatazo.

  1. Bainisha matumizi au mahitaji yako ya msingi na yasiyo ya msingi. Aina na kiwango cha matumizi hutofautiana mtu na mtu, sehemu anapoishi na shughuli za uchumi anazofanya. Kwa mfano, matumizi ya mwajiriwa anayeishi kwenye nyumba ya kukodi jijini Daressalaam na kutumia usafiri wa daladala kila siku kwenda kazini ni tofauti na mjasiriamali nje ya jiji la Mwanza, anayeishi kwenye nyumba yake yenye bustani au shamba. Lisha ya tofauti hizo, matumizi yafuatayo yanaweza kukupatia mwongozo wa kupata picha ya matumizi yako: (i) Chakula, (ii) Kodi ya Nyumba, (iii) Nishati, kama vile umeme, gesi, mkaa, (iv) Gharama za Shule/Karo, (v) Mavazi, (vi) Usafi binafsi, k.v. Sabuni na vipodozi, (vii) Vifaa vya nyumbani, (viii) Bima ya afya, (ix) Mengineyo (nauli, mawasiliano, michango, burudani n.k.).

Unaweza kufupisha au kurefusha orodha hii kulingana na mahitaji yako binafsi. Kubainisha gharama halisi ulizonazo kila mwezi hukusaidia kuyaoanisha na mapato yako ya mwezi na kuhakikisha unamudu mahitaji na majukumu yako ya msingi bila shida huku ukiendelea na mipango yako ya kimaendeleo. Iwapo una mipango ya kuwekeza mahala fulani au kujikusanyia mtaji, pesa inayobaki kutoka kwenye matumizi unaweza kuitenga kila mwezi bila kuathiri hadhi au kiwango chako cha maisha. Ni wazi kuwa, kama kipato chako hakitoshi kukidhi mahitaji ya msingi, huna budi kutathmini matumizi yako na kuyapunguza au kutafuta kazi yenye kipato kinachoendana na gharama zako za maisha.

  1. Weka Akiba kwa ajili ya dharura. Dharura haipangwi, bali hujitokeza yenyewe. Na kuna dharura zinazokulenga moja kwa moja, ambazo hauwezi kukwepa, kama vile matibabu, uharibifu wa mali au kupoteza kazi/kipato. Akiba hii, ambayo hukadiriwa kuwa sawa na kipato chako cha miezi mitatu mpaka sita, ni tofauti na pesa unayoitenga katika kuwekeza katika biashara. Hii ni kwa sababu biashara yako ikiyumba, inaweza kukulazimu uchukue pesa kutoka katika mahitaji yako ya msingi na hivyo kushindwa kumudu gharama za maisha. Njia mojawapo ya kukwepa ukali wa dharura ni kuwa na Bima ya afya. Kutegemea na aina ya kifurushi utakachochukua, bima ya afya inakuwezesha kupunguza hatari ya kuichumi inayotokana na dharura ya kuugua. Kwa kulipia bima ya afya kutokana na pesa uliyoipangalia kwenye matumizi yako kila mwezi, unapata matibabu bila ya kuathiri akiba yako. Kwa mtu mwenye familia au mwenye ndugu anayehitaji matibabu ya mara kwa mara, kulipia bima ya afya sio tu ni kuwekeza kwenye afya bali ni tendo lenye uwajibikaji mkubwa, hasa katika dharura ya matibabu au pale unaposhindwa kulipia matibabu makubwa. Kulingana na utafiti wa FInscope (2017), matumizi ya matibabu yanashika nafasi ya tatu kwa umuhimu (baada ya gharama za kuishi, yaani chakula, kodi/malazi) na dharura ya kiafya/matibabu ni sababu namba moja ya watu kokopa pesa na kuingia kwenye madeni.
  2. Kuwa jasiri kuwekeza. Kuwekeza husaidia kujiongezea uwezo wako kuichumi na hukusaidia kutimiza malengo yako nje ya mahitaji yako ya kila siku. Sio kila mtu anaweza kuwa mfanya biashara mashuhuri, hasa ukiwa umeajiriwa wakati huo huo (kumbuka: ni hatari kuacha ajira iwapo biashara yako haikupi kipato cha kutimiza mahitaji ya kila siku). Tambua kipaji chako na wekeza katika talanta yako kupitia shughuli unayoiwezea vizuri. Badala ya biashara, unaweza kuboresha au kukuza bustani/shamba lako na ukajipunguzia gharama za chakula, kupata akiba ya chakula au hata kuuza na kupata fedha kwa ajili ya mipango mingine. Wengine hufuga, wengine husuka, wengine hujenga vibanda au nyumba kwa ajili ya kupangisha. Mianya ni mingi unapopata nafasi ya kujihabarisha na kubadilishana mawazo na watu. Walisiliana nasi pia kwa mawazo zaidi.

Kuna usemi usemao: „Mtu hula kulingana na urefu wa kamba yake“. Kuna hekima katika kutathmini matumizi binafsi, kujiongezea uwezo wa kipato, bila kuhatarisha mahitaji binafsi au ya familia, na kukwepa mikopo au utegemezi. Baadhi ya watu wanamudu hili jambo bila shida, wengine hupata ugumu. Iwapo unahitaji msaada zaidi, kimawazo au ushauri, usisite kujereja kwetu kupitia mawasiliano yalioko mwishoni mwa ukurasa huu. Tutafurahi sana   kukusaidia.

Barikiwa.

 

Bibliografia

Finscope Tanzania (2017). Insights that drive Innovation. https://www.fsdt.or.tz/wp-content/uploads/2017/09/Finscope.pdf

 

Namna ya Kufanikiwa katika Biashara Unayoianzisha

Kuanzisha biashara Tanzania huambatana na changamoto kadhaa kama ukosefu wa mtaji na mkakati dhaifu wa uuzaji. Lakini badala ya kuangalia sababu zinazofanya biashara kushindwa, napenda tujikite katika makala hii kwenye mambo yanayoweza kufanikisha biashara inayoanzishwa. Mawazo haya nimeyagawanya katika dondoo zifuatazo.

Tazama biashara za maeneo jirani unayoishi au biashara za watu unaowafahamu. Je, ni mambo gani yaliyofanya biashara hizo kufanikiwa, kubaki vilevile kwa muda mrefu, au hata kushindwa? Ni sababu zipi zimeleteleza matokeo hayo?

Kwa hakika kuna sababu nyingi,  zikiwemo sababu binafsi ambazo ziko nje ya uewelewa wetu. Kwa msingi huo hatuwezi tukadai kujua sababu za kila biashara kushindwa. Hata hivyo, napenda tutazame baadhi ya mambo muhimu yanayopelekea biashara kufanikiwa au hata kushindwa.

  1. Mkakati dhabiti wa uuzaji. Watanzania wanafahamu kutumia fursa katika kufanya biashara zao. Hii huusisha kufungua biashara katika maeneo yalio na watu wengi, au karibu ya kaya zao ambapo wanaweza kuduhumia kaya za jirani kwa bidhaa na huduma huku wakitimiza majukumu yao ya nyumbani. Popote pale biashara yako ilipo, ili ikue na ifanikiwe, inapaswa kujikita katika kutimiza hitaji flani la watu walioko katika eneo hilo.  Hivyo shauku ya kuanzisha biashara na kujishughulisha haina budi kuambatana na mahitaji ya msingi ya watu katika eneo husika. Ili kuweza kujua mahitaji ya wateja wako wa baadaye na kufanya uamuzi mzuri wa aina ya biashara ya kuendesha, unapaswa kufanya utafiti wa soko.
  2. Naamini unafahamu tabia ya baadhi ya watu kuelekea katika fursa flani ya biashara na kubadili mwelekeo, yaani biashara, pale wanapoona fursa nyingine. Ni kweli kuwa kupata uzoefu katika biashara tofauti tofauti huleta manufaa. Hata hivyo, swala la kubadili badili biashara lapaswa kutathminiwa kwa kina, hasa pale ambapo matokeo yake yanaathiri kipato cha familia. Kwa hakika jambo hili tunalitazama kwa utofauti, iwapo mtu ana kipato thabiti kutokana na ajira, chenye kukidhi mahitaji yake na familia yake huku “akijijaribu” katika biashara flani. Kutimiza wajibu wa riziki yako na familia yako ni muhimu huku ukijikita katika biashara yako kwa uvumilivu na kutafuta mafanikio katika biashara hiyo.
  3. Udhibiti mzuri wa mtaji. Nimekutana na baadhi ya wanafanyabiashara wanaotumia pesa au bidhaa za biashara kwa ajili ya matumizi yao binafsi (k.v. kwa ajili chakula, nauli au dharura). Hili jambo, hata kama wakati flani halikwepeki, linahitaji nidhamu kubwa. Ikarimu unaweza kuhatarisha biashara yako. Kutenganisha matumizi ya biashara na matumizi binafsi ni jambo la msingi sana. Ni kweli kuwa upatikanaji wa mtaji ni muhimu katika kuanzisha biashara. Mtu achukuaye mkopo kwa ajili ya mtaji anapaswa kutuambua deni analodaiwa na umuhimu wa kulipa deni hilo, ukizingatia kuwa kipindi cha awali cha biashara huwa kinaambatana na hasara. Kiasi kikubwa cha mkopo humaanisha pia kiasi kikubwa cha deni na kiasi kikubwa cha deni huweza kupelekea kushindwa kulipa kama pesa haidhibitiwi vizuri au ikijitokeza hasara kubwa kutoka na mauzo au wizi. Kama unakusudia kuanzisha biashara ndogo, fikiria kuhusu biashara zisizohitaji mtaji au zinazohitaji mtaji mmdogo. Kumbuka methali inayosema: “Mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe” . Jipatie mawazo kupitia mtandao au marafiki kuhusu aina za biashara zisizohitaji mkopo au zinazohitaji mkopo mdogo. Unaweza kuwasiliana nasi kwa mawazo zaidi.
  4. Jifunze kuboresha biashara yako. Kimsingi, ni vema kupata maarifa ya biashara hata kabla ya kuanza biashara. Unaweza kuona wepesi wa kufanya biashara, lakini kuwa mnyenyekevu ili kujifunza zaidi na kuepuka makosa ya kibiashara, kunaweza kukusogeza mbele zaidi. Kama umeshaanza biashara yako, jipatie muda, utoke katika mihangaiko ya biashara yako, ili ujifunze namna ya kuiboresha. Kutana na wanafanyabiashara wengine wazoefu zaidi na waliofanikiwa, pata ushauri kutoka benki, jiunge katika jukwaa la majidala au tafuta mshauri wa kitaalam ili ujifunze kutokana na uzoefu wa wengine na changamoto zao. Unaweza kufaidika sana.

Je, kuna mambo mengine ya kuzingatia katika kuendesha biashara? Tafadhali tushirikishe. Kama una swali au haja yoyote, jiskie huru kuwasiliana nasi. Kama inahitaji kufahamu zaidi kuhusu uendeshaji wa biashara, jipatie nyenzo hapa.

Nakutakia kila la kheri katika biashara yako

Umuhimu wa Kujiendeleza Kielimu

Kazi nyingi siku hizi zinahitaji elimu, iwe ni kwa mtu anayeingia soko la ajira, au anapoanza biashara, au kwa mtu anayehitaji kuboresha utendaji wake katika taaluma au kazi anayoifanya. Hata hivyo, kutokana na ushindani uliopo katika soko la kazi na mategemeo yaliyowekwa katika ubora wa utendaji kazi, haina budi kila mtu kujiendeleza kitaaluma. Mtu aliyesoma, kubobea katika taaluma yake, na kujipatia uzoefu wa kazi hata  katika kipindi cha uanafunzi katika kujitolea mahali, ana fursa kubwa ya kujitengenezea riziki kwa ajili yake na familia yake. Katika ngazi zote za elimu, Tanzania inatoa fursa ya kujiendeleza kielimu na kubobea katika fani au taaluma. Jedwali lifuatalo linaonesha baadhi masomo ya taaluma tofauti tofauti katika kiwango cha cheti na stashahada. Asilimia kubwa ya kozi hizi huweza kusomwa na mtu aliyehitimu elimu ya sekondari (kidato cha nne). Jedwali hili ni mfano tu unaoweka bayana kuwa kila mtu (katika kiwango chake cha elimu) anaweza kujiendeleza na kubobea katika taaluma anayopenda. Tofauti na kuanza moja kwa moja na elimu ya cheti au stashahada, kuna uwezekano wa bobea kwenye taaluma kupitia VETA, shahada au hata kozi fupi zinazotelea na taasisi tofauti tofauti za elimu. Kama una maswali zaidi au unahitaji ushauri kuhusiana na kujiendeleza kielimu, wasiliana nasi kupitia mawasiliano yetu yalioko upande wa chini wa ukurasa huu. Ili kuziona kozi ya cheti na stashahada, bonyeza hapa.

Mwongozo wa Usajili wa Biashara kwa Mitaji Midogo na Mikubwa

 

Unatamani kuanzisha biashara yako ili uweze kutimiza njozi yako ya maisha na kujitegemea kiuchumi?

Ni dhahiri kuwa sio kila mtu anaweza kufanya biashara yoyote. Huenda umesha litafakari hili na kufanya tathmini kuhusu aina ya biashara inayoendana na uwezo na karama yako. Huenda pia umeshajipatia uzoefu katika biashara yako hiyo na kutathmini soko lake. Kama sivyo, usisite kuwasiliana nasi ili tuweze kuangalia kwa pamoja ni biashara ipi inaweza kukufaa na nambna ya kijipatia taarifa na mafunzo muhimu kwa ajili ya biashara hiyo.

Waraka huu unakusudia kukupatia mwongozo mfupi wa hatua unazopaswa kuzichukua kabla ya kuanzisha biashara yako. Hii inakusaidia kuzingatia miongozo muhimu ya kisheria ili kuweza kuanzisha biashara yako iliyo rasmi, itakayokufungulia milango ya huduma zingine maalumu, k.v. mkopo wa benki, mafunzo, na mtandao wa wafanyabiashara wengine. Hata hivyo waraka huu unakusaidia kukupa tathmini fupi ya gharama zinazohusika katika kupanga na kuanzisha biashara yako.

Hatua za uanzishaji wa biashara:
– Hatua ya kwanza ni lazima ujue aina ya biashara unayohitaji kuanzisha, ikiwemo na rasilimali husika (k.v. ofisi, pikipiki, elimu husika/cheti, bima n.k.). Uamuzi wa aina ya biashara huhusisha pia uamuzi kama biashara hiyo itaendeshwa kama biashara ya mtu binafsi, ubia au kampuni yenye dhima ya ukomo

– Hatua ya pili ni kusajili jina la biashara yako katika ofisi ya BRELA (Mamlaka ya Usajili wa Biashara na Leseni). Gharama utakayolipa kwa ajili ya hati ya usajili ni Tsh. 20 000/-

– Hatua ya tatu ni kupata namba ya mlipakodi (TIN). Namba hii utaipata katika ofisi ya TRA ya Mkoa au Wilaya baada ya kujaza fomu ya maombi ya namba ya utambulisho wa mlipakodi. Namba ya TIN ni bure, ila utalipia ushuru kutokana na makadirio yako ya mapato ya mwaka huo au mtaji wako uliowekeza katika biashara

– Hatua ya nne ni kujipatia leseni ya biashara katika ofisi za biashara katika wilaya, manispaa, jiji au wizara ya biashara na viwanda. Gharama ya leseni hutegemea aina ya biashara unayohitaji kuanzisha. Gharama hii utaijua katika ofisi hiyo ya biashara. Kutazama fomu ya maombi ya leseni, bonyeza hapa.

Bajeti ya gharama zote za kupitia hatua hapo juu ili kuanzisha biashara ya mtu binafsi (kwa mfano) hukadiriwa kuwa shilingi laki tatu (Tsh. 300 000/-). Kwa mtu ambaye hana uwezo wa kulipa hii pesa, anashauriwa kurejea katika mfumo wa wafanyabiarasha/wajasiriamali wadogo na kujipatia kitambulisho kutoka katika ofisi za TRA kabla ya kuanzisha biarasha yake. Ili kuweza kufanikisha ili, unapaswa kuanzia na taratibu husika katika serikali zako za mitaa. Jifahamishe katika eneo unaloishi kuhusiana na uwepo wa mifumo hii vikundi au umoja wa biashara fulani fulani zinazoweza kukupatia msaada zaidi. Fomu ya maombi ya kitambulisho cha mjasiriamali unaweza kuipakua hapa. Gharama ya kitambulisho cha mjasiriamali mdogo ni Tsh. 20 000/-

Kama una swali ama unahitaji mwongozo zaidi, usisite kuwasiliana nasi kupitia info@societalnurturing.com au 0784462140