Fursa ya Mikopo bila Riba kwa ajili ya Biashara

Je, wajua kuwa unaweza kupata bila riba kwa ajili ya kuendesha shughuli zako za kiuchumi? Basi endelea kusoma makala hii kupata taarifa zaidi.

Hivi karibuni, Halmashauri zote za Tanzania zimeweka mkazo katika kutoa mikopo isiyokuwa na riba kwa makundi maalum kama vile wanawake, vijana (miaka 18 -35), na watu wenye ulemavu. Hii imefanyika kwa kutoa asilimia kumi ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa kila kundi, huku wanawake wakipewa asilimia nne, vijana asilimia nne, na watu wenye ulemavu asilimia mbili. Hatua hii inalenga kuchochea ujasiriamali na maendeleo ya kiuchumi katika makundi haya, huku ikiondoa kabisa gharama ya riba.

ZIFUATAZO NDIO VIGEZO VYA KUSTAHIKI KUPATA MKOPO:

Ili kustawisha kutolewa kwa mikopo isiokuwa na riba, kuna vigezo muhimu ambavyo kundi linalokusudiwa kupata mkopo linapaswa kukidhi. Hii ni hatua muhimu kuhakikisha kwamba mikopo inawafikia wale wanaoihitaji na inachangia katika maendeleo ya ujasiriamali na shughuli za kiuchumi. Hapa chini ni orodha ya vigezo hivyo: Kumbuka, vigezo hivi ni kwa Halmashauri zote za Tanzania.

Ujasiriamali na Nia ya Kuanzisha Shughuli za Kiuchumi: Kundi linapaswa kuonyesha jitihada za kujishughulisha katika ujasiriamali au kuwa na nia ya kuanzisha shughuli za kiuchumi.

Ukubwa wa Kundi: Kwa vikundi vya wanawake au vijana, linapaswa kuwa na wanachama kumi au zaidi. Kwa upande wa watu wenye ulemavu, vikundi visiwe chini ya watano wala kuzidi kumi. Hii inalenga kuwahusisha wengi iwezekanavyo katika fursa hii.

Akaunti ya Benki: Kundi linapaswa kuwa na akaunti ya benki kwa jina la kikundi. Hii ni hatua muhimu katika usimamizi wa fedha na kudumisha uwazi katika matumizi ya mikopo.

Ukosefu wa Ajira Rasmi: Wanachama wa kikundi wasiwe na ajira rasmi. Hii inasisitiza lengo la mikopo isiokuwa na riba kusaidia wale ambao wanaweza kukosa ufikiaji wa mikopo kwa njia za kawaida.

Raia wa Tanzania na Umri: Wanachama wanapaswa kuwa raia wa Tanzania wenye umri wa miaka kumi na nane au zaidi. Hii inahakikisha kwamba mikopo inawalenga wale ambao wana haki ya kisheria kuingia mikataba ya kifedha.

MAOMBI YA MKOPO:

kikundi kinachotamani kupata mkopo kitapaswa kuanza safari yake kwa kujaza fomu maalum ya maombi. Fomu hii itatolewa na Halmashauri husika. Baada ya kujaza kwa makini fomu ya maombi, hatua muhimu inayofuata ni kuambatisha nyaraka zinazounga mkono ombi. Hii ni hatua ya muhimu katika kuhakikisha ufanisi wa mchakato wa maombi. Kwa mfano, kikundi kinahitajika kuambatanisha nakala za katiba yake, cheti cha usajili wa kikundi, na, ikiwa kinafanya biashara, leseni ya biashara.

Vilevile, ni muhimu kutoa nakala halisi za taarifa za akaunti kutoka benki ambayo kikundi kina akaunti. Hii itathibitisha utaratibu wa kifedha wa kikundi. Barua za utambulisho kutoka kwa Mtendaji wa Kijiji au Mtaa pamoja na Mtendaji wa Kata zinahitajika kama uthibitisho wa uwepo wa kikundi katika eneo husika. Pia, kutoa wazo la biashara kunahitajika kueleza kwa kina shughuli za biashara ambazo kikundi kinataka kutekeleza. Halmashauri itakuwa mshirika wa karibu katika mchakato huu. Baada ya kupokea maombi, Halmashauri ina jukumu la kutoa taarifa ya kupokea ombi hilo kwa kikundi husika ndani ya siku tatu. Hii ni hatua muhimu inayowawezesha waombaji kujua kuwa hatua yao ya kwanza imefanikiwa.

Muda wa Kushughulikia Maombi ya Mikopo: Halmashauri imechukua jukumu la kuhakikisha mchakato wa maombi ya mikopo unakamilika kwa ufanisi na haraka. Kipindi cha kushughulikia maombi hakitaenda zaidi ya miezi mitatu tangu siku ya kupokelewa kwa maombi hayo. Kwa kuongezea, jukumu la Halmashauri halimalizi tu na kushughulikia maombi. Wanachukua hatua ya ziada kuhakikisha fedha zinaelekezwa mahali sahihi. Mara tu vikundi vinapokidhi vigezo na kusaini mkataba wa makubaliano, Halmashauri ina jukumu la kupeleka fedha hizo kwa haraka katika akaunti za vikundi husika.

Marejesho: Mkopo uliotolewa kwa kikundi utatakiwa kuanza kurejeshwa baada ya muda wa miezi mitatu tangu siku ya kupata mkopo. Hii inamaanisha kuwa vikundi vitapewa muda wa “grace period” kama wanavyosema wamombo wa miezi mitatu bila kulazimika kuanza marejesho. Baada ya kipindi hiki, vikundi vitahitajika kuanza mchakato wa kurejesha mikopo yao kwa mujibu wa makubaliano. Muda huu wa miezi mitatu unalenga kuwapa wakopaji muda wa kuanzisha au kuimarisha shughuli zao za biashara kabla ya kuanza kurejesha mkopo. Hii ni hatua inayosaidia kuhakikisha kwamba vikundi vinapata fursa ya kujipanga kifedha na kuepuka shinikizo la malipo mapema.

HITIMISHO

Kupitia mpango huu wa mikopo bila riba, wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu wana fursa mpya zenye manufaa makubwa. Faida za mpango huu ni dhahiri, kwani unawawezesha kujenga biashara zako bila mzigo wa riba, huku ukipata mtaji wa kuanzia. Hii sio tu inakupa nguvu za kifedha, bali pia inaleta ufanisi katika jamii kwa kuchochea ujasiriamali na maendeleo ya kiuchumi. Fursa hii inawawezesha kuchangia katika ukuaji wa jamii  na kuwa nguvu inayosukuma mbele ustawi wa pamoja. Tembelea Halmashauri yako kwa taarifa na ushauri zaidi.

Iwapo utahitaji msaada katika kupata mkopo huu, hususan katika kuandika katiba au mpango wa biashara, karibu uwasiliane nasi. Iwapo tayari umeshapata mkopo huu, tutafurahi kusikia kuhusu uzoefu wako. Kama unahitaji kuboresha biashara yako ili kuimarisha kipato na kujihakikishia kiwango cha marejesho ya mkopo, tutafurahi kushiriki kukusogeza hatua nyingine ya mafanikio

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *