Namna ya Kufanikiwa katika Biashara Unayoianzisha

Kuanzisha biashara Tanzania huambatana na changamoto kadhaa kama ukosefu wa mtaji na mkakati dhaifu wa uuzaji. Lakini badala ya kuangalia sababu zinazofanya biashara kushindwa, napenda tujikite katika makala hii kwenye mambo yanayoweza kufanikisha biashara inayoanzishwa. Mawazo haya nimeyagawanya katika dondoo zifuatazo.

Tazama biashara za maeneo jirani unayoishi au biashara za watu unaowafahamu. Je, ni mambo gani yaliyofanya biashara hizo kufanikiwa, kubaki vilevile kwa muda mrefu, au hata kushindwa? Ni sababu zipi zimeleteleza matokeo hayo?

Kwa hakika kuna sababu nyingi,  zikiwemo sababu binafsi ambazo ziko nje ya uewelewa wetu. Kwa msingi huo hatuwezi tukadai kujua sababu za kila biashara kushindwa. Hata hivyo, napenda tutazame baadhi ya mambo muhimu yanayopelekea biashara kufanikiwa au hata kushindwa.

  1. Mkakati dhabiti wa uuzaji. Watanzania wanafahamu kutumia fursa katika kufanya biashara zao. Hii huusisha kufungua biashara katika maeneo yalio na watu wengi, au karibu ya kaya zao ambapo wanaweza kuduhumia kaya za jirani kwa bidhaa na huduma huku wakitimiza majukumu yao ya nyumbani. Popote pale biashara yako ilipo, ili ikue na ifanikiwe, inapaswa kujikita katika kutimiza hitaji flani la watu walioko katika eneo hilo.  Hivyo shauku ya kuanzisha biashara na kujishughulisha haina budi kuambatana na mahitaji ya msingi ya watu katika eneo husika. Ili kuweza kujua mahitaji ya wateja wako wa baadaye na kufanya uamuzi mzuri wa aina ya biashara ya kuendesha, unapaswa kufanya utafiti wa soko.
  2. Naamini unafahamu tabia ya baadhi ya watu kuelekea katika fursa flani ya biashara na kubadili mwelekeo, yaani biashara, pale wanapoona fursa nyingine. Ni kweli kuwa kupata uzoefu katika biashara tofauti tofauti huleta manufaa. Hata hivyo, swala la kubadili badili biashara lapaswa kutathminiwa kwa kina, hasa pale ambapo matokeo yake yanaathiri kipato cha familia. Kwa hakika jambo hili tunalitazama kwa utofauti, iwapo mtu ana kipato thabiti kutokana na ajira, chenye kukidhi mahitaji yake na familia yake huku “akijijaribu” katika biashara flani. Kutimiza wajibu wa riziki yako na familia yako ni muhimu huku ukijikita katika biashara yako kwa uvumilivu na kutafuta mafanikio katika biashara hiyo.
  3. Udhibiti mzuri wa mtaji. Nimekutana na baadhi ya wanafanyabiashara wanaotumia pesa au bidhaa za biashara kwa ajili ya matumizi yao binafsi (k.v. kwa ajili chakula, nauli au dharura). Hili jambo, hata kama wakati flani halikwepeki, linahitaji nidhamu kubwa. Ikarimu unaweza kuhatarisha biashara yako. Kutenganisha matumizi ya biashara na matumizi binafsi ni jambo la msingi sana. Ni kweli kuwa upatikanaji wa mtaji ni muhimu katika kuanzisha biashara. Mtu achukuaye mkopo kwa ajili ya mtaji anapaswa kutuambua deni analodaiwa na umuhimu wa kulipa deni hilo, ukizingatia kuwa kipindi cha awali cha biashara huwa kinaambatana na hasara. Kiasi kikubwa cha mkopo humaanisha pia kiasi kikubwa cha deni na kiasi kikubwa cha deni huweza kupelekea kushindwa kulipa kama pesa haidhibitiwi vizuri au ikijitokeza hasara kubwa kutoka na mauzo au wizi. Kama unakusudia kuanzisha biashara ndogo, fikiria kuhusu biashara zisizohitaji mtaji au zinazohitaji mtaji mmdogo. Kumbuka methali inayosema: “Mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe” . Jipatie mawazo kupitia mtandao au marafiki kuhusu aina za biashara zisizohitaji mkopo au zinazohitaji mkopo mdogo. Unaweza kuwasiliana nasi kwa mawazo zaidi.
  4. Jifunze kuboresha biashara yako. Kimsingi, ni vema kupata maarifa ya biashara hata kabla ya kuanza biashara. Unaweza kuona wepesi wa kufanya biashara, lakini kuwa mnyenyekevu ili kujifunza zaidi na kuepuka makosa ya kibiashara, kunaweza kukusogeza mbele zaidi. Kama umeshaanza biashara yako, jipatie muda, utoke katika mihangaiko ya biashara yako, ili ujifunze namna ya kuiboresha. Kutana na wanafanyabiashara wengine wazoefu zaidi na waliofanikiwa, pata ushauri kutoka benki, jiunge katika jukwaa la majidala au tafuta mshauri wa kitaalam ili ujifunze kutokana na uzoefu wa wengine na changamoto zao. Unaweza kufaidika sana.

Je, kuna mambo mengine ya kuzingatia katika kuendesha biashara? Tafadhali tushirikishe. Kama una swali au haja yoyote, jiskie huru kuwasiliana nasi. Kama inahitaji kufahamu zaidi kuhusu uendeshaji wa biashara, jipatie nyenzo hapa.

Nakutakia kila la kheri katika biashara yako

One Reply to “Namna ya Kufanikiwa katika Biashara Unayoianzisha”

Leave a Reply to Agatha Cancel reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *