Lengo la makala hii ni kukuwezesha kuanza biashara mara moja na kuifanikisha, iwapo utaamua. Hivyo karibu uisome makala hii mpaka mwisho.
Kama inavyofahamika, swala la mtaji, ujuzi, usimamizi mzuri na kutambua/kutengeneza fursa ni misingi muhimu katika uendeshaji wa biashara. Mara nyingi biashara zinakwama katika msingi hii. Hebu tafakari jambo hili:
Fundi anapokuwa anashidwa kuhakikisha kazi ya mteja imefanyika wa uzuri na kwa wakati, huathiri kipato chake na ukuaji wa biashara yake. Mategemeo ya faida ya haraka na ukosefu wa nidhamu katika matumizi ya pesa ya biashara, hupelekea kutumia sehemu ya pesa ya biashara katika mahitaji binafsi (k.v. matibabu, chakula, ada ya shule) au hata kupunguza kuwekeza muda wa kutosha katika biashara. Katika mazingira haya, biashara hubaki kuwa duni.
Huenda umeshafirikia ni biashara gani ungependa kuianzisha na vigezo unavyohitaji kuvitimiza ili kufanikisha biashara hiyo. Umetathimini soko na kuona kuna fursa au uhitaji mkubwa ya bidhaa au huduma unayotaka kuitoa na pesa unayolenga kuipata. Kanuni iongozayo ni uhitaji wa bidhaa au huduma yako. Kama hakuna uhitaji mkubwa, hiyo biashara haiwezi ikajiendesha na kukidhi mahitaji yako. Panapokuwa na uhitaji mkubwa, una uhakika wa wateja. Wakati mwingine inakuhitaji kujihakishia wateja wa awali na kuwa na mzunguko mdogo wa pesa ili kuimarisha biashara yako, kabla haujabobea katika hiyo biashara na kuwekeza muda na pesa zaidi, au hata kusitisha shughuli zako zingine.
Biashara nyingi zinahitaji mtaji, ila sio zote. Kwa mfano biashara zinazotumia ujuzi wako na sisizohitaji ofisi kama, kufundisha au kusuka, hazihitaji mtaji. Hivyo, tafakari kuhusu gharama unazoweza kuziepuka katika kuanzisha biarashara yako.
Ujuzi wa kazi katika bishara ni muhimu. Mwalimu anayefundisha shule haitaji kufahamu utaratibu wa makato ya serikali, vibali na gharama za uendeshaji, namna ya kupata na kuwafikia wateja na kutengeneza mfumo mzuri wa uendeshaji wa kituo au kutengeneza mikataba. Mwalimu anayeendesha kituo cha tuisheni kwa upande mwingine hupaswa kufahamu haya. Hivyo unapoanzisha biashara yako, tafakari kuhusu mambo unayopaswa kuyajua kabla ya kuanza.
Je, katika biashara unayokusudia na una ujuzi wa kutosha? Unahitaji ujuzi kuhusu namna ya kujipatia wateja na kukuza biashara yako kupitia mtandao? Ni kweli, si lazima ujue kila kitu ili uanze biashara ila unapaswa kutambua mipaka yako katika kufikia malengo uliyoweka. Kupitia mafunzo, marafiki, washauri au hata wafanyabiashara wenza, unaweza kuziba hilo pengo.
Ili kufikia malengo, usimamizi unapaswa kuwa mzuri. Usimamizi huusisha mipango ya muda mfupi na mrefu. Pamoja na namna ya kufikia malengo hayo, juhudi na usimamizi katika kufikia malengo hayo, watu/wafanyakazi watakaosaidia kufika malengo hayo, uongozi na ukaguzi wa kazi, pamoja na maamuzi thabiti pale ambapo malengo husika hayajafikiwa, ni mambo ya msingi ya kuzingatia.
Pale ambapo unakuwa hauko makini katika kutimiza malengo ya biashara, kutoweka mbinu za kutimiza kazi hata wakati wa dharura, lazima kutambua athari yake katika biashara na kipato chako. Unapochagua ndugu au marafiki kama wafanyakazi bila kuweka kipaumbele katika uwezo na elimu yao, bila kuzingatia mgongano wa masilahi katika kukamilisha malengo yako ya biashara na kupata ujuzi unaohitaji, ni rahisi kuwa na biashara isiyoendelea. Sio lazima kumuajiri mtu na kufanya kazi naye, ili uweze kumsaidia. Biashara nyingi za kusaidiana zinabaki katika hali ya chini, hazikidhi gharama ya uendeshaji na mahitaji. Wengi wanaishia kuomba omba na kukopa, lisha ya kuwa wana biashara. Kuna watu wanaokubali tenda ili wapate pesa ya kufanya kazi ya mteja mwingine na kupata hela ya kula. Mazingira haya yamefanya biashara zetu nyingi kuwa katika hali duni.
La mwasho – biashara nyingi hushindwa kufanyika kwa sababu ya kusingizia vikwazo vya mtaji, ujuzi au mifumo duni (sheria n.k.). Visingizio hivi havisaidii pale tunapotafuta suluhisho hata kwa kuanza taratibu.
Mfano: kama ninahitaji kufungua stationery na sina mtaji wa milioni 3 au siwezi kupata kwa ndugu/marafiki, naweza kuona pa kuanzia huku nikiweka mpango thabiti namna ya kufikia lengo hilo, hata kama likichukua muda zaidi. Naweza nikaangalia pa kuanzia kulingana na mahitaji ya wateja hali nikijua sitaweza kuitegemea hiyo biashara riziki ya kila siku. Mahitaji ya wateja yaweza kuwa madaftari, kalamu, nitanunua vitu hivyo na kuuzia wateja huku huku nikiendelea kuzingatia mahitaji zaidi na kukuza mtaji wangu. Naweza pia kutumia Kompyuta ya mtu kuchapa kazi za wateja. Njia hii ndefu ni uwekezaji, haupaswi kutegemewa kama riziki, lakini husadia kufikia malengo
Mfano wa pili: Kama ninahitaji pikipiki kama kitega uchumi ila sina hela, naweza
- Kuunganisha nguvu na mtu/watu (njia ya haraka)
- Kukusanya pesa taratibu kwa ajili ya pikipiki nitakayoimudu baadaye
- Kuchagua biashara mbadala yenye mtaji nitakaomudu, ila wenye matapo yatakayoniwezesha kuelekea kwenye hilo lengo la pikipiki
Iwapo unahitaji msaada zaidi katika kuanzisha na kushimamisha biashara yako, usisite kuwasiliana nasi.