Namna ya kumudu gharama zako za maisha

Nani havifahamu vipindi vya hali ngumu kiuchumi ambapo unajikuta kipato chako hakitoshi kutekeleza mipango ulionayo au hata matumizi yako ya muhimu. Hasa pale dharura zinapozitokeza, k.v. matibabu, uharibifu wa mali za msingi au kupoteza kazi/kutolipwa mshahara, ni rahisi kujikuta katika changamoto kubwa ya kukidhi mahitaji binafsi. Mtu mwenye utamaduni wa kujiwekea akiba ya kutosha hata kuweza kumudu kipindi cha miezi kadhaa cha dharura au mtu mwenye vipato mbadala kutoka katika miradi mingine anaweza kuwa katika nafasi nzuri ya kumudu dharura hizi huku akiendeleza mipango yake ya maisha na ya maendeleo. Kwa sababu si wote walio na akiba au miradi hii, lazima tutazame njia zingine za kuweza kumudu gharama za maisha ambazo zaweza kufungua njia mbadala za kujihakikishia akiba. Ili kurahisisha usomaji, nimeyafupisha mawazo yangu katika dondoo zifuatazo.

  1. Bainisha matumizi au mahitaji yako ya msingi na yasiyo ya msingi. Aina na kiwango cha matumizi hutofautiana mtu na mtu, sehemu anapoishi na shughuli za uchumi anazofanya. Kwa mfano, matumizi ya mwajiriwa anayeishi kwenye nyumba ya kukodi jijini Daressalaam na kutumia usafiri wa daladala kila siku kwenda kazini ni tofauti na mjasiriamali nje ya jiji la Mwanza, anayeishi kwenye nyumba yake yenye bustani au shamba. Lisha ya tofauti hizo, matumizi yafuatayo yanaweza kukupatia mwongozo wa kupata picha ya matumizi yako: (i) Chakula, (ii) Kodi ya Nyumba, (iii) Nishati, kama vile umeme, gesi, mkaa, (iv) Gharama za Shule/Karo, (v) Mavazi, (vi) Usafi binafsi, k.v. Sabuni na vipodozi, (vii) Vifaa vya nyumbani, (viii) Bima ya afya, (ix) Mengineyo (nauli, mawasiliano, michango, burudani n.k.).

Unaweza kufupisha au kurefusha orodha hii kulingana na mahitaji yako binafsi. Kubainisha gharama halisi ulizonazo kila mwezi hukusaidia kuyaoanisha na mapato yako ya mwezi na kuhakikisha unamudu mahitaji na majukumu yako ya msingi bila shida huku ukiendelea na mipango yako ya kimaendeleo. Iwapo una mipango ya kuwekeza mahala fulani au kujikusanyia mtaji, pesa inayobaki kutoka kwenye matumizi unaweza kuitenga kila mwezi bila kuathiri hadhi au kiwango chako cha maisha. Ni wazi kuwa, kama kipato chako hakitoshi kukidhi mahitaji ya msingi, huna budi kutathmini matumizi yako na kuyapunguza au kutafuta kazi yenye kipato kinachoendana na gharama zako za maisha.

  1. Weka Akiba kwa ajili ya dharura. Dharura haipangwi, bali hujitokeza yenyewe. Na kuna dharura zinazokulenga moja kwa moja, ambazo hauwezi kukwepa, kama vile matibabu, uharibifu wa mali au kupoteza kazi/kipato. Akiba hii, ambayo hukadiriwa kuwa sawa na kipato chako cha miezi mitatu mpaka sita, ni tofauti na pesa unayoitenga katika kuwekeza katika biashara. Hii ni kwa sababu biashara yako ikiyumba, inaweza kukulazimu uchukue pesa kutoka katika mahitaji yako ya msingi na hivyo kushindwa kumudu gharama za maisha. Njia mojawapo ya kukwepa ukali wa dharura ni kuwa na Bima ya afya. Kutegemea na aina ya kifurushi utakachochukua, bima ya afya inakuwezesha kupunguza hatari ya kuichumi inayotokana na dharura ya kuugua. Kwa kulipia bima ya afya kutokana na pesa uliyoipangalia kwenye matumizi yako kila mwezi, unapata matibabu bila ya kuathiri akiba yako. Kwa mtu mwenye familia au mwenye ndugu anayehitaji matibabu ya mara kwa mara, kulipia bima ya afya sio tu ni kuwekeza kwenye afya bali ni tendo lenye uwajibikaji mkubwa, hasa katika dharura ya matibabu au pale unaposhindwa kulipia matibabu makubwa. Kulingana na utafiti wa FInscope (2017), matumizi ya matibabu yanashika nafasi ya tatu kwa umuhimu (baada ya gharama za kuishi, yaani chakula, kodi/malazi) na dharura ya kiafya/matibabu ni sababu namba moja ya watu kokopa pesa na kuingia kwenye madeni.
  2. Kuwa jasiri kuwekeza. Kuwekeza husaidia kujiongezea uwezo wako kuichumi na hukusaidia kutimiza malengo yako nje ya mahitaji yako ya kila siku. Sio kila mtu anaweza kuwa mfanya biashara mashuhuri, hasa ukiwa umeajiriwa wakati huo huo (kumbuka: ni hatari kuacha ajira iwapo biashara yako haikupi kipato cha kutimiza mahitaji ya kila siku). Tambua kipaji chako na wekeza katika talanta yako kupitia shughuli unayoiwezea vizuri. Badala ya biashara, unaweza kuboresha au kukuza bustani/shamba lako na ukajipunguzia gharama za chakula, kupata akiba ya chakula au hata kuuza na kupata fedha kwa ajili ya mipango mingine. Wengine hufuga, wengine husuka, wengine hujenga vibanda au nyumba kwa ajili ya kupangisha. Mianya ni mingi unapopata nafasi ya kujihabarisha na kubadilishana mawazo na watu. Walisiliana nasi pia kwa mawazo zaidi.

Kuna usemi usemao: „Mtu hula kulingana na urefu wa kamba yake“. Kuna hekima katika kutathmini matumizi binafsi, kujiongezea uwezo wa kipato, bila kuhatarisha mahitaji binafsi au ya familia, na kukwepa mikopo au utegemezi. Baadhi ya watu wanamudu hili jambo bila shida, wengine hupata ugumu. Iwapo unahitaji msaada zaidi, kimawazo au ushauri, usisite kujereja kwetu kupitia mawasiliano yalioko mwishoni mwa ukurasa huu. Tutafurahi sana   kukusaidia.

Barikiwa.

 

Bibliografia

Finscope Tanzania (2017). Insights that drive Innovation. https://www.fsdt.or.tz/wp-content/uploads/2017/09/Finscope.pdf

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *