Mwongozo wa Usajili wa Biashara kwa Mitaji Midogo na Mikubwa

 

Unatamani kuanzisha biashara yako ili uweze kutimiza njozi yako ya maisha na kujitegemea kiuchumi?

Ni dhahiri kuwa sio kila mtu anaweza kufanya biashara yoyote. Huenda umesha litafakari hili na kufanya tathmini kuhusu aina ya biashara inayoendana na uwezo na karama yako. Huenda pia umeshajipatia uzoefu katika biashara yako hiyo na kutathmini soko lake. Kama sivyo, usisite kuwasiliana nasi ili tuweze kuangalia kwa pamoja ni biashara ipi inaweza kukufaa na nambna ya kijipatia taarifa na mafunzo muhimu kwa ajili ya biashara hiyo.

Waraka huu unakusudia kukupatia mwongozo mfupi wa hatua unazopaswa kuzichukua kabla ya kuanzisha biashara yako. Hii inakusaidia kuzingatia miongozo muhimu ya kisheria ili kuweza kuanzisha biashara yako iliyo rasmi, itakayokufungulia milango ya huduma zingine maalumu, k.v. mkopo wa benki, mafunzo, na mtandao wa wafanyabiashara wengine. Hata hivyo waraka huu unakusaidia kukupa tathmini fupi ya gharama zinazohusika katika kupanga na kuanzisha biashara yako.

Hatua za uanzishaji wa biashara:
– Hatua ya kwanza ni lazima ujue aina ya biashara unayohitaji kuanzisha, ikiwemo na rasilimali husika (k.v. ofisi, pikipiki, elimu husika/cheti, bima n.k.). Uamuzi wa aina ya biashara huhusisha pia uamuzi kama biashara hiyo itaendeshwa kama biashara ya mtu binafsi, ubia au kampuni yenye dhima ya ukomo

– Hatua ya pili ni kusajili jina la biashara yako katika ofisi ya BRELA (Mamlaka ya Usajili wa Biashara na Leseni). Gharama utakayolipa kwa ajili ya hati ya usajili ni Tsh. 20 000/-

– Hatua ya tatu ni kupata namba ya mlipakodi (TIN). Namba hii utaipata katika ofisi ya TRA ya Mkoa au Wilaya baada ya kujaza fomu ya maombi ya namba ya utambulisho wa mlipakodi. Namba ya TIN ni bure, ila utalipia ushuru kutokana na makadirio yako ya mapato ya mwaka huo au mtaji wako uliowekeza katika biashara

– Hatua ya nne ni kujipatia leseni ya biashara katika ofisi za biashara katika wilaya, manispaa, jiji au wizara ya biashara na viwanda. Gharama ya leseni hutegemea aina ya biashara unayohitaji kuanzisha. Gharama hii utaijua katika ofisi hiyo ya biashara. Kutazama fomu ya maombi ya leseni, bonyeza hapa.

Bajeti ya gharama zote za kupitia hatua hapo juu ili kuanzisha biashara ya mtu binafsi (kwa mfano) hukadiriwa kuwa shilingi laki tatu (Tsh. 300 000/-). Kwa mtu ambaye hana uwezo wa kulipa hii pesa, anashauriwa kurejea katika mfumo wa wafanyabiarasha/wajasiriamali wadogo na kujipatia kitambulisho kutoka katika ofisi za TRA kabla ya kuanzisha biarasha yake. Ili kuweza kufanikisha ili, unapaswa kuanzia na taratibu husika katika serikali zako za mitaa. Jifahamishe katika eneo unaloishi kuhusiana na uwepo wa mifumo hii vikundi au umoja wa biashara fulani fulani zinazoweza kukupatia msaada zaidi. Fomu ya maombi ya kitambulisho cha mjasiriamali unaweza kuipakua hapa. Gharama ya kitambulisho cha mjasiriamali mdogo ni Tsh. 20 000/-

Kama una swali ama unahitaji mwongozo zaidi, usisite kuwasiliana nasi kupitia info@societalnurturing.com au 0784462140

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *